Mbunge wa Mtera Livingstone Lusinde amewapiga marufuku wabunge wa CCM kukikosoa chama hicho ndani ya Bunge kwa kuwatahadharisha wao si wasemaji wa chama na wapo watu waliochaguliwa kufanya hivyo na amesema hayo kama 'bosi' wao.
Lusinde ametoa kauli hiyo jana bungeni katika mjadala wa bajeti ya Serikali mwaka 2018/19, baada ya baadhi ya wabunge kutoka majimbo ya mikoa ya kusini kuonyesha hofu ya CCM kushindwa katika uchaguzi mkuu ujao kutokana na serikali kuamua kubadili sheria ya korosho ili kuwezesha mapato yote yatokanayo na ushuru wa korosho inayosafirishwa nje kuingizwa mfuko mkuu wa serikali bila kugawanya.
Lusinde amewataka wabunge kama hawatakuwa na lugha sahihi ya kukosoa au kusifia ni vyema wakatulia kuliko kufanya shughuli zinazopaswa kufanywa na watu wengine.
“Humu ndani tunapochangia tujiepushe na kazi za wengine. Eti tukifanya hivi tutashindwa sisi si wasemaji wa chama. Sisi wabunge wa CCM kazi yetu ni kuisimamia Serikali, kukosoa na kuitetea na nasema kama bosi wenu humu ndani ni marufuku kwa mbunge wa CCM kukizungumzia chama humu,” alisema.
“Hiki ni chama chenye Serikali na tupo hapa kuisimamia si kuikosoa CCM. Kauli za kuiweka chama kwenye hatari ya kushinda au kushindwa si sehemu yake hapa. Tunavyo vikao vya kukosoana tuataambiana huko. Kama wabunge wangu hamna lugha ya kuisifia na kuikosoa nyamazeni kimya, ”
Lusinde amedai kwamba ametoa onyo hilo siyo kama Mbunge tu bali kama mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho.
Pamoja na hayo akichangia kuhusu mjadala wa korosho uliokuwa unaendelea ndani ya bunge Lusinde amewataka wabunge kama ni kusimamia ukweli wote wanapaswa kusimamia ukweli na kama ni mabadiliko basi yafanywe kwa kuzingatia sheria.
No comments:
Post a Comment