SERIKALI imepeleka sh.
bilioni 2.6 katika Jiji la Mwanza kwa ajili ya kugharamia uboreshaji wa vituo
vya afya ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Hayo yalibainika jana (Jumanne, Februari 20, 2018) wakati Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa alipokagua na kuweka jiwe la msingi la kituo cha afya cha
Karume.
Waziri Mkuu alikagua ukarabati wa kituo hicho kilichopo kwenye
kata ya Bugogwa wilayani Ilemela akiwa katika siku ya sita ya ziara yake
ya kikazi mkoani Mwanza.
Alisema uboreshaji huo ulihusisha ujenzi wa chumba cha upasuaji,
maabara, chumba cha kujifungulia, jengo la mama na mtoto na wodi ya wanawake na
wanaume.
Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na uboreshaji wa kituo hicho,
ambapo Serikali inatarajia kupeleka sh. milioni 200 kwa ajili ya ununuzi wa
vifaa mbalimbali.
Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha inasogeza huduma za
afya karibu na wananchi. Uboreshaji wa kituo cha afya cha Karume umegharimu
takriban sh. milioni 497 hadi hivi sasa.
Waziri Mkuu aliongeza kuwa mkakati wa Rais Dkt. John
Magufuli ni kuimarisha sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata
matibabu karibu na maeneo yao ya makazi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndungulile alisema Serikali imetoa sh.
bilioni 2.6 kwa ajili ya uboreshaji wa vituo vya afya jijini Mwanza.
Alisema fedha hizo zinalenga kuboresha vituo hivyo ili
kuviwezesha kutoa huduma bora kwa wananchi wa jiji zikiwemo huduma za afya ya
mama na mtoto, upasuaji na maabara.
Awali, Waziri Mkuu alifungua zahanati ya Bulale iliyopo katika
kata ya Buhongwa wilayani Nyamagana na kisha alitoa vitambulisho vya matibabu
kwa wazee 250. Jumla ya wazee 5,398 wilayani humo wamepatiwa vitambulisho vya
matibabu.

No comments:
Post a Comment